Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imefanya ukaguzi wa Ghala za kuhifadhia na Vituo vya kujazia Gesi ya kupikia (LPG).
Ukaguzi huo umefanyika katika Kampuni ya LAKE GAS iliyopo Machui Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na Kampuni ya ORYX iliyopo Masingini Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha huduma ya gesi inahifadhiwa kwa kuzingatia ubora na usalama, pia kuhakikisha ujazaji wa gesi unazingatia viwango vilivyowekwa kwa mitungi ya kilo 6, kilo 15 na kilo 32.
Aidha, ZURA imezitaka kampuni hizo kuhakikisha mitungi hiyo inasambazwa na inapatikana kwa kiwango kinachohitajika katika maeneo ya mjini na vijijini Unguja na Pemba.
Pia ukaguzi huo ulijikita katika kukagua usalama wa wafanyakazi kwenye mazingira yao ya kazi, vitendea kazi ikiwemo viatu na kofia ngumu, pia ukaguzi huo uliangalia iwapo ghala za gesi zilizokaguliwa zinapitisha hewa ya kutosha na zina vifaa vya kuzimia moto.
ZURA hufanya ukaguzi wa uingizaji, uhifadhi, ujazaji, usambazaji na uuzaji wa gesi kwa kuangalia ubora wa bidhaa na miundombinu ya gesi mara kwa mara Unguja na Pemba ili kuimarisha huduma ya gesi na kuhakikisha huduma hiyo inatolewa katika hali ya usalama zaidi.

